VICHWA vya mashabiki wa Simba viko ‘bize’ sana wakati huu. Hiki wanachokiona kwa Ibrahim Ajib, mbele ya mboni zao kinatisha mno. Ni kama wanatazama sinema ya kutisha ambayo hawakujiandaa nayo. Simba wanajua ubora wa Ajib, lakini hakuna kati yao aliyetegemea angekuwa hatari kiasi hiki. Awali walikuwa na maneno machache sana pindi wanapomwelezea Ajib. Kijana mwenye kipaji, lakini mvivu wa mazoezi. Hivyo tu. Lakini kwa sasa ukitamka Ajib, unamzungumzia mfalme wa Yanga. Unamzungumzia mmoja kati ya wachezaji hatari zaidi kwenye VPL. Ajib huyu wa Yanga, ni kiumbe tofauti kabisa na yule aliyeondoka Msimbazi, huku wenyewe wakitabasamu. Huyu wa sasa ni mpambanaji anayewalazimisha mabeki watii amri zake. Ni ujuha kwa mchezaji wa aina yake, kuendelea kumwita mvivu wa mazoezi. Nini kimembadilisha Ajib? Nitakwambia. Ipi tofauti ya Ajib wa Simba na huyu wa Yanga? Nitakwambia pia. Kwa sasa acha nikueleze kwanini Simba wanatakiwa kuwa makini na Ajib, jioni ya Oktoba 28. Moja katika mabadiliko makubwa ya kiufundi yaliyofanywa na kocha wa Yanga, George Lwandamina, ni kuyabadilisha majukumu ya Ajib uwanjani. Awali alikuwa akimtumia kama mshambuliaji anayetokea pembeni. Nafasi aliyokuwa akiicheza mara kwa mara alipokuwa Simba. Anapamudu, lakini huwa na mapungufu baadhi kwenye eneo hilo. Kwanza huwa hakabi. Pili ana vitu vingi vya kufanya na mpira kabla hajafanya maamuzi ya kupiga pasi. Madhara ya mambo haya mawili, ni pale anapopokonywa mpira. Timu pinzani huwa kwenye nafasi nzuri ya kumpa shida mlinzi wa pembeni. Tuliona nyakati fulani, Gadiel Michael, alivyokuwa akipata shida kucheza kwenye mstari mmoja na Ajib. Nini Lwandamina alifanya? Kumsogeza Ajib nyuma ya straika. Kuanza kumpanga kama namba 10. Hapa amekuwa huru zaidi. Amekuwa msuka mipango wa timu. Uwezo wake wa kumiliki mpira na kupiga chenga, umekuwa faida kwa Yanga na tishio kwa wapinzani anaokutana nao. Sishangai Obrey Chirwa anavyonufaika na huduma za Ajib. Sitashangaa pia Amissi Tambwe, akirudi na kuingia kwenye orodha ya wagombea kiatu cha ufungaji bora. Kucheza mbele ya Ajib, unahitaji uwe unajua kazi moja tu. Kufunga. Benchi la ufundi la Simba lina kazi ya ziada ya kuhakikisha linamdhibiti Ajib. Na pengine wasifanikiwe pia kama Kamusoko na Tshishimbi watabaki kwenye ubora wao tuliozoea. Kumdhibiti Ajib aliye na mpira mguuni ni kazi ngumu kama kumdhibiti Mange Kimambi, mwenye bando la intaneti kwenye simu yake. Lazima atakiwasha tu. Huyu Ajib wa Yanga ni mkomavu. Anacheza kwa sababu ya matokeo na si kulifurahisha jukwaa. Na Yanga wamefanikiwa hili kwa sababu ile ile ambayo Simba huwa wanafanikiwa mara zote kwa Emmanuel Okwi. Kumwamini mchezaji. Yanga wanamwamini sana Ajib. Walimkaribisha kifalme Jangwani. Wakaheshimu kipaji chake na wakasimama nyuma yake wakimshangilia. Simba hawakuwahi kumhesabu Ajib kuwa miongoni mwa wafalme wao. Alipofunga, walishangilia. Alipokosea, wakarudia neno lao lile lile ‘mvivu’. Ni kama wanavyofanya sasa kwa Mohammed Ibrahim. Ni kama Yanga wanavyofanya sasa kwa Mwinyi Haji. Naamini tumeelewana. Kama ambavyo wengi tumekuwa tukimshangaa Ajib. Tukishangaa mabao yake na juhudi zake uwanjani. Nawahakikishia viongozi wa Simba nao wako kwenye hali hiyo hiyo. Bahati mbaya hawawezi kukiri hili hadharani. Kwa sasa wamebaki na swali moja kichwani lenye majibu mawili moyoni. Siwasemei na siko tayari kuwajibia, ila nilicho na uhakika nacho kwa sasa, mashabiki wa Simba, wameshajua kwanini Ajib anaitwa ‘miguu ya dhahabu’. Omog ashangilie kwanza mabao manne ya Yanga ACHANA na beki wa Yanga atakayepewa jukumu la kumkaba Okwi. Sahau pia kiungo wa Simba, atakayekuwa na jukumu la kucheza na Papy Tshishimbi. Mwanadamu mwenye siku ngumu zaidi ikifika Oktoba 28, ni Joseph Omog. Ni siku ngumu sana kwake. Pengine siku ngumu kuliko zote katika maisha yake ya ukocha. Ni siku hii matokeo ya uwanjani yatakapoamua hatima ya kibarua chake. Sote tunajua kinachoendelea ndani ya Simba wakati huu. Mashabiki hawana imani na Omog. Hawaridhishwi na kiwango cha kikosi chao. Kitu pekee kinachombakisha Omog Simba mpaka leo hii ni busara za viongozi wa klabu hiyo. Tunaelekea Oktoba 28. Simba wanachotaka ni ushindi mbele ya Yanga. Hakuna hadithi nyingine. Na wa kwanza anayewajibika na hili ni Joseph Omog. Sawa. Omog hana namna ya kukwepa zigo hili. Ni lazima alibebe jukumu na kuhakikisha anawapa furaha Wanasimba. Kitu cha kwanza Omog anachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuinua mikono juu kwa Mungu na kushukuru kwa ushindi walioupata Yanga mbele ya Stand United. Kwanini? Lingekuwa jambo gumu sana kucheza na Yanga ile isiyojiamini. Angekuwa kwenye presha kubwa mno ya kimaandalizi. Lakini sasa Yanga wamerudi kwenye mstari. Ushindi wa mabao manne utawafanya waingie katika pambano na Simba wakijiamini. Kitu hiki kimeifanya presha ya mchezo isiwe upande wake pekee. Mchezo umerudi na kusimama katikati. Hakuna anayeweza kuutabiri. Anaweza kutulia na kupanga silaha zake kwa utulivu. Umakini wa viongozi umeongezeka pia. Kila mmoja anajua wanakwenda kucheza na Yanga iliyo imara. Ni tofauti na mwanzo alivyokuwa akijiandaa kucheza na Yanga, iliyoonekana kuchoka. Ingeweza kumpotezea umakini, lakini sasa kila kitu kiko sawa.

0 comments :
Post a Comment