News
Loading...
Image Map HII NI 24 RADIO SIKILIZA NA UTUTUMIE SMS KWENDA 0684 666320 KUHUSU UNAVYOTUSIKIA

Saturday, 28 October 2017

UCHAMBUZI WA MECHI A SIMBA vs YANGA:"UFUNDI" MBINU" VIKOSI" USHAURI


Yanga dhidi ya Simba ni moja ya michezo mikali ambayo ungeweza kuifikiria ambayo pengine inachangiwa na ubora wa vikosi vyenyewe, ubora na mbinu za makocha lakini pia historia ya vilabu hivi viwili ndani ya soka la Tanzania. Utakuwa mchezo ambao kila kocha atakuwa anajaribu kujiweka karibu au jirani na msimamo ulivyokuwa kwa ujumla wake.

George Lwandamina

Wengi wanaweza kuwa wanadharau sababu za kocha huyu kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wake kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliopita dhidi ya Stand United. Lakini Lwandamina alijua ratiba yake, alifahamu fika akiwaruhusu wachezaji wake wacheze huenda wakapata kadi za njano, nyekundu au majeraha yatakayoifanya ratiba yake kuwa ngumu zaidi. Ndio maana alichagua kuwa huru, kumweka benchi Juma Abdul na Kelvin Yondani kwa kuwa hii ndio mihimili yake iliyoshikilia ngome yake ya ulinzi tangu kuanza kwa msimu.
George Lwandamina akifuatilia mchezo wa dhidi ya MCA ( Picha/ Soka360)
Lwandamina anajua Simba sio Stand United. Ugumu wa Simba ni wachezaji wake wa eneo la katikati mwa uwanja na mbele ambao wote ni kama wapo huru na wanaweza kuhamisha eneo lako la ulinzi watakavyo. Kwa eneo la ulinzi ni tofauti, kuna wakati huruhusu makosa ya kizembe kama lile dhidi ya Stand United, kipa anaokoa hatari, mabeki wanatazamana kuuondosha mpira ingawa maendeleo yanaonekana kadri siku zinavyokwenda.
Lwandamina atatakiwa kuziba mianya ya Erasto Nyoni ambaye ni mpishi mzuri tu ndani ya kikosi cha Simba. Kichwa pengine kitakuwa kinauma zaidi akimfikiria Emmanuel Okwi, na si ajabu akaanza na mbinu za kuhakikisha Okwi hatembei wala kuivuka kingo ya eneo lake la hatari, lakini mtu ambaye anaweza kuwa hatari zaidi ni Mzamiru Yassin ambaye hutumika kama mshambuliaji wa pili ndani ya makaratasi huku uwanjani akicheza kama mshambuliaji nambari moja endapo Okwi atakabwa na kutoruhusiwa kutembea.

Joseph Omog

Makocha Mecky Mexime wa Kager Sugar na Joseph Omog wa Simba wakipeana mikono wakati wa pamabano la kwanza mwaka jana.
Ushindi mnono dhidi ya Njombe Mji unaweza kuwa umempa amani kubwa ya moyo hasa katika mfumo wake wa 4-3-3. Kulikuwa na mtiririko mzuri wa kiuchezaji kwa timu yake na uwepo wa Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Mzamiru Yassin umempa namna mpya ya kiuchezaji ambayo inaongeza mashambulizi zaidi.
Kichwani kwake atakuwa anawaza makosa machache ya safu yake ya ulinzi dhidi ya uwepo wa Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib. Lakini timu yake imepata muda mwingi wa kutulia sehemu tulivu na kurudisha zile kumbukumbu za siku kama hii inavyokuwa.

Mbinu, Yanga

Yanga wanaonekana wataendelea kutumia mfumo wa 4-3-3. Huu mfumo unamaanisha kuwa mzigo wa ubunifu utakuwa mgongoni kwa Papy Kabamba muda mwingi huku wakitegemea kasi ya Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa kuweza kuitawanya falsafa ya ulinzi ya Joseph Omog. Uzuri wa huu mfumo ni kuwa unamfanya Donald Ngoma muda mwingi kuwa katika nafasi sahihi mipira inapokuwa inakuja kwake, maana pembeni wachezaji wapo.
Papy Kabamba na Rafael Daud wanaonekana kuendelea kutengeneza umoja kwenye eneo la katikati mwa uwanja kiulinzi na kimashambulizi. Hii ni silaha nyingine ya Yanga, na inaweza kuwabeba leo hasa kama Omog ataamua kumtumia James Kotei kwa sababu hakutakuwa na ubunifu mkubwa ambao utawafungua watu kirahisi.

Mbinu, Simba

Jonas Mkude ni ongezeko ambalo linampa Joseph Omog uhai katikati mwa uwanja. Mkude anajua kutulia na mpira na upokonyaji wake umekuwa mzuri sana kipindi hiki. Bahati kwake ni kuwa anaweza kuwa anakutanmuda na Rafael Daud muda mwingi ambaye hana kasi na si mwepesi kuliko Thabani Kamusoko. Dhidi ya Njombe Mji ilikuwa rahisi kwa sababu kazi nyingi za Njombe Mji zilifanyika katikati mwa uwanja ambako ndipo Mkude hupendelea kucheza. Lakini bado anahitajika kuifanya Simba ishinde mapambano katikati mwa uwanja.
Haruna Niyonzima ni jemedari mwingine atayekuwa ameshilkilia bendera ya vita kwenye mchezo huu, usimwangalie kwa jicho la kawaida, huyu ni mtaalamu wa pasi zenye ustadi na usahihi pia huifanya timu kushambulia kwa kasi kubwa, akilini mwake tukio huanza kuliona na kisha ndipo huja kulitenda. Ni mzuri wa kucheza mipira yote inayohusiana na sanaa, na hii huweza kuwasababishia kadi wachezaji wa Yanga.

Mkude dhidi ya Daud, Kamusoko

Kichwa kinaweza kuwa kinauma hapa kwa Lwandamina. Binafsi ningemchagua Kamusoko kisha nimrudishe Rafael Daud nyuma akacheze na Papy kama viungo wawili wa ulinzi huku nikitumia mifumo miwili uwanjani, ule mama wa 4-3-3 na ule wa uongo wa 4-2-3-1 timu inapokuwa ikishambuliwa kwa sababu Simba si Stand United wala Mtibwa Sugar. Hawa hawana ubunifu mkubwa katikati mwa uwanja. Ili uwaweze unatakiwa kuwa na ubunifu kidogo tu na utulivu. Lakini Lwandamina anaweza kuamua kumchukua Rafael Daud kwa sababu anamuamini tangu msimu huu kuanza licha ya uzoefu kuwa ndio changamoto kubwa kwake kwenye ratiba hii.

Mchezo wa faida

Kama Omog ataanzisha 4-2-3-1 kisha ndani wakawepo James Kotei na Jonas Mkude basi itabidi awaagize wakabe sana pembeni. Kuzuia muunganiko wa Ajib na Chirwa, hawa sio kazi ndogo kwa mabeki wa pembeni. Hawa wote wana kasi kubwa ambayo inaweza kuwa tatizo hasa kama Simba wataruhusu mipira ya krosi kwa Chirwa huyu ambaye yupo kwenye kiwango bora.
Yanga wao watamuhitaji Papy Kabamba aliyecheza dhidi ya Lipuli. Asikimbie sana uwanjani lakini aondoe uhuru kwa washambuliaji wa Simba, awaondoe Niyonzima na Mzamiru katika uwiano wao kisha apenyeze mipira inayotakiwa kuanzisha mwendo kwa timu. Yanga itamtegemea Ajib awe hatari na ili ulinzi wa Simba upungue nguvu. Akifanya kazi yake vyema maana yake ni kuwa hata walinzi, Juma Abdul na Gadiel Michael watakuwa sawa na wataongeza presha vyema.

Ninachofikiri

Hautokuwa mchezo kama wa Simba dhidi ya Njombe Mji au Yanga dhidi ya Stand United. Hawa wote watatamani kupunguza kasi ya vilabu vingine kwenye msimamo wa ligi.
Lwandamina na Omog watakuwa na nafasi kubwa ya kufanya vyema kutokana na kupumzika muda mwingi lakini pia itategemea na kwa kiasi gani wachezaji wao watacheza vyema eneo la kati ili kupunguza presha kwenye penalti boksi.
Omog atataka Okwi afunge, na hili litawezekana kama hatocheza mbali na boksi ya Yanga kwani Andrew Vincent na Kelvin Yondani hawana muunganiko mzuri, wana makosa yanayojirudia sana, hasa ya kukosa maelewano nani awe mlinzi wa mwisho au nani akabe eneo. Halidi Abdulrahman.
USISAHAU KULIKE PAGE YETU HAPA
Share on Google Plus

About

0 comments :

Post a Comment