SIMBA ilikuwa inachonga sana kwa madai kuwa inamiliki ukuta wote wa Taifa Stars, lakini mambo yamebadilika gafla na kuna dalili hayatarudi kama ilivyokuwa awali.
Miezi miwili iliyopita Simba ilikuwa na wachezaji; Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Abdi Banda na Shomary Kapombe, katika kikosi cha kwanza cha Stars, lakini beki mkongwe wa Yanga, Kelvin Yondani ametibua kila kitu.
Yondani ametibua mchongo wa Simba katika kikosi hicho cha Stars baada ya kurejea na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza akimuweka benchi Mbonde.
Katika mchezo wa juzi Jumamosi wa kirafiki dhidi ya Botswana, Erasto Nyoni ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyecheza katika safu ya ulinzi ya Stars huku nafasi nyingine zikichezwa na Gadiel Michael wa Yanga na Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini.
Simba ilikuwa imejihakikishia nafasi zote za ulinzi katika kikosi cha Stars, lakini kurejea kwa Yondani ambaye amekuwa nje ya timu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, kumeharibu mambo.
Yondani ambaye amewahi kuichezea Stars kwa miaka 10, alirejeshwa katika kikosi hicho kwa mara nyingine na kucheza dakika zote 90 dhidi ya Botswana ambapo Stars ilishinda kwa mabao 2-0.
Awali nafasi hiyo ilishikiliwa na Salim Mbonde na Erasto Nyoni ambao wote ni wa Simba.
Mabeki wengine wa Simba, Kapombe ni majeruhi huku Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akishindwa kuitwa kwa kuwa hajawa fiti tangu atoke kuuguza majeraha ya enka.
Akizungumzia kurejea kwa Yondani katika kikosi cha Stars, nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta, alisema beki huyo bado ana kiwango cha juu na anastahili kuendelea kulitumikia taifa.
“Ni mchezaji mkubwa, anacheza vizuri na ameonyesha kiwango cha maana. Naweza kusema anatakiwa kuendelea kuwa hapa,” alisema Samatta.
“Alistahili kuwepo kabla, pengine kocha alikuwa anafanya tu mzunguko wa wachezaji, lakini kwa Yondani hakuna ubishi,” aliongeza nyota huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji.
Kwa upande wa kocha wa Stars, Salum Mayanga, alisema alipanga kumtumia Yondani kwenye mechi za kufuzu Chan, lakini alishindwa kutokana na nyota huyo kuwa kwenye majukumu ya ndoa.
“Nilipozungumza naye alisema ana majukumu ya ndoa, nisubiri kwanza, nadhani sasa tunakwenda vizuri,” alisema.

0 comments :
Post a Comment