Mwanza. Mashabiki wa Simba Mwanza wamesema ushindi wa mabao 4-0 waliopata dhidi ya wenzao wa Yanga ni ishara tosha kuwa timu yao itashinda katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 23.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Buhongwa, mabao ya timu ya mashabiki wa Simba yalifungwa na Philip Tzeba dakika ya 18, Andrea Mathina (44), Nduya Delick (69) na Delick Deogratias ( 79).
Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa kuazimisha siku ya Simba Day, mashabiki hao wametamba kuwa Simba ni timu bora.
Kariba Paulo, shabiki ndaki ndaki wa Simba aliyendaa mchezo huo alisema aliamua kuwakutanisha mashabiki wa Simba na Yanga kufurahia siku hiyo.
Alisema kushinda mchezo huo ni ishara ya ushindi wa Simba katika Ngao ya Jamii na Ligi Kuu baada ya kufanya usajili bora.
"Huu mchezo ulikuwa maalumu kwa wana Simba na Yanga katika kuazimisha siku ya Simba Day, kwahiyo tutaendelea kuungana sisi kama watani" alisema Paulo.



0 comments :
Post a Comment