BEKI wa Mbao FC, Yussuph Ndikumana, amesema kuwa yupo tayari kujiunga na Yanga katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo ili kuungana na kocha wake, Ettiene Ndayiragije anayetajwa kuwa mbioni kurithi mikoba ya Mzambia George Lwandamina.
Ndayiragije amekuwa akitajwa kuchukua nafasi ya Lwandamina baada ya klabu hiyo kutoridhishwa na mwenendo wa timu yao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Habari za Ndayiragije kutua Yanga, zilienea tangu mwanzoni mwa wiki hii ambapo ilidaiwa kuwa kocha huyo raia wa Burundi, alionekana jijini Dar es Salaam ambako alikutana na mabosi wa mabingwa hao wa Tanzania Bara na kuwapa sharti la kuwa kocha mkuu na si msaidizi.
Hata hivyo, Ndayiragije alipoulizwa juu ya taarifa hizo, alikana kukutana na kiongozi yeyote wa Yanga, lakini akiweka wazi kuwa yupo tayari kutua Jangwani iwapo atatakiwa na kukubaliana na klabu hiyo katika suala zima la masilahi.
Akifahamu kuwa kuna uwezekano wa Ndayiragije kutua Yanga, Ndikumana aliliambia BINGWA kuwa iwapo mpango huo utafanikiwa, basi mashabiki wa Wanajangwani hao wajiandae kumpokea.
“Ni kweli Yanga walinitaka, wakala wangu aliwasikiliza lakini hakuridhika na dau ambalo walitaka kunipa, nina imani Ndayirangije akiondoka na kujiunga na Yanga, kwangu itakuwa rahisi kuungana naye huko,” alisema Ndikumana.
Beki huyo king’ang’anizi anayeibeba Mbao FC, alisema anatamani kumwona Ndayiragije akijiunga na Wanajangwani hao hata leo ili naye aweze kutimiza ndoto za baba yake mzazi za kuitumikia Yanga.
Baba mzazi wa Ndikumana amekuwa ni shabiki mkubwa wa Yanga ambapo wakati timu hiyo ilipokuwa ikimfuatilia, mwanaye wakati wa usajili wa dirisha kubwa, alikuwa na furaha kubwa lakini ghafla kijana wake huyo aliyeyuka Jangwani.
Sababu ya Ndikumana kushindwa kusajiliwa Yanga baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, ni baada ya wakala wake kushindwana dau la usajili na mshahara na uongozi wa klabu hiyo.


0 comments :
Post a Comment