NA EZEKIEL TENDWA
KAMA ulidhani Jonas Mkude anavyokalishwa benchi pale Simba anapenda, utakuwa unakosea kwani ni kutokana na ushindani wa namba uliopo na sasa huenda hali hiyo ikamkumba hata Haruna Niyonzima, endapo atajisahau na kutegea mazoezi, kutokana na kasi aliyokuja nayo Mghana, Nicholas Gyan.
Mkude ambaye ilikuwa nadra sana kumkosa kikosi cha kwanza, sasa hivi anasugulishwa benchi akiwashuhudia akina James Kotei na Mzamiru Yassin, wakimfunika na sasa Niyonzima naye akiteleza tu kidogo, Gyan anampeleka benchi ambapo kitu pekee kitakachomnusuru Mnyarwanda huyo na hali hiyo, ni kukaza buti.
Simba wamemsajili Gyan, kutoka katika timu ya Ebusua Dwarfs ya nchini Ghana na mchezo wake wa kwanza ulikuwa wa tamasha la ‘Simba Day’ dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, uliomalizika kwa wekundu wa Msimbazi hao kuibuka na ushindi wa bao 1-0, ambapo licha ya kinda huyo kuingia kipindi cha pili, aliuwasha moto kisawasawa.
Baada ya mchezo huo alirejea kwao Ghana kumalizana na timu yake kitu kilichosababisha kukosa michezo miwili ule wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, na ule wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting na alipowasili tu hakutaka maneno mengi badala yake alianza mazoezi mara moja na kuonekana mchezo wa kirafiki dhidi ya Hard Rock ya Pemba.
Katika mchezo huo ambao Simba walishinda mabao 5-0, Gyan ambaye aliingia kipindi cha pili alionyesha uwezo mkubwa na kufanikiwa kufunga bao moja ambapo kutokana na kasi aliyonayo mchezaji yeyote atakayezubaa akiwamo Niyonzima, anaweza kujikuta aking’olewa kikosi cha kwanza.
Mbali na Niyonzima, pia John Bocco, naye hayupo salama sana kwani akilemaa benchi linaweza likamhusu na hata Shiza Kichuya naye hali ni hiyo hiyo, kwani mbali na kucheza kama mshambuliaji, pia Gyan, anamudu vema nafasi ya winga huyo ikimaanisha kwamba ushindani wa namba Simba hautamwacha mtu salama.
Hata katika mazoezi ambayo Simba wanafanya wakijiwinda na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Jumamosi ya wiki hii, Gyan anaonekana amekuja kikazi zaidi kutokana na namna anavyojituma na haitashangaza akianzishwa kikosi cha kwanza mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex
* USISAHAU KULIKE PAGE YETU HAPA*

0 comments :
Post a Comment