NIMEUONA mtazamo wa mashabiki wengi wa soka nchini juu ya Azam FC. Wengi wanaamini ya safari hii Azam sio timu imara tena.
Imani imetoweka kabisa kwa mashabiki baada ya nyota kadhaa wa timu hiyo wakiwamo Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Gadiel Michael na John Bocco kuondoka pale Chamazi.
Mashabiki wengi wa soka wanaamini msimu huu Azam itakuwa timu ya kusindikiza wengine tu. Hata hivyo kwa hili tutakuwa tunajidanganya, Azam bado si timu ya kubeza.
Nimeitazama Azam katika mechi za kirafiki hapa nyumbani na kule Uganda na kubaini kwamba bado ni timu ya kuwania ubingwa. Bado ina kikosi bora cha kwanza na kikosi kizuri cha akiba.
Ukiachana na mechi za awali ambazo Azam ilichezesha watoto wengi, mechi za majuzi kule Uganda zimetoa picha ya tofauti kabisa. Azam imecheza mechi tano ndani ya siku nane ilizokaa Uganda, haikupoteza hata mchezo mmoja. Si jambo dogo.
Ilicheza na timu ya taifa ya Uganda inayoshiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) na kutoa sare. Ikacheza na mabingwa wa Uganda, KCCA na kutoa sare pia. Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara kisha wakatia timu kwenye mechi dhidi ya URA, Vipers na Onduriparaka, hizo ilishinda zote.
Jambo kubwa ambalo limeonekana katika mechi za Azam ni uimara wa safu ya ulinzi na ile ya ushambuliaji. Katika mechi hizo tano, Azam imeruhusu mabao matatu tu, lakini imefunga mara tisa.
Ni kiwango bora hasa kwa timu iliyokwenda kucheza ugenini. Kufunga mabao tisa katika mechi tano ni sawa na wastani wa mabao mawili katika kila mchezo, kama timu inafanya vizuri kwenye ulinzi ni wazi kwamba kwa namba hiyo ni ngumu kupoteza mechi.
Wakati huo ikifunga mabao tisa bado safu yake ya ushambuliaji haijatimia. Azam bado inawakosa Mbaraka Yusuf na Shaaban Iddi katika safu hiyo.
Hakuna asiyefahamu ubora wa Mbaraka wala Iddi. Msimu uliopita Mbaraka alifunga mabao 12 kwenye Ligi Kuu Bara akizidiwa mawili tu na wafungaji bora; Simon Msuva na Abdulrahman Mussa.
Msimu uliopita Shaban Iddi alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Vijana kabla ya kuwa mfungaji bora namba mbili katika timu yake ya Azam. Shaaban Iddi na Mbaraka wote walitwaa tuzo msimu uliopita.
Hapa sasa unaweza kuona upana uliopo katika safu ya ushambuliaji ya Azam. Yahya Mohammed sasa anaonekana kuwa katika ubora wake. Uwezo wake wa kufunga umeimarika tofauti na msimu uliopita. Chipukizi Yahya Zaidi naye anaonekana kuimarika na kuonyesha uwezo. Nyota wengine Waziri Junior na Joseph Kimwaga pia bado wapo vizuri. Ni wazi kwamba safu hii inaendelea kuwa na makali.
Safu ya kiungo ya Azam bado ipo vizuri. Himid Mao bado yupo kwenye ubora wa juu. Frank Domayo na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ bado wako vizuri. Akina Bryson Raphael, Mkameruni Stephan Kingue na chipukizi Abdallah Masoud bado wako vizuri.
Kwa tathmini ya haraka ni kwamba kwa timu za Ligi Kuu Bara, baada ya Simba, Azam ndiyo ina safu ngumu ya kiungo. Kwa sasa Simba ndiyo timu yenye viungo bora zaidi nchini, hilo halina ubishi.
Kwenye safu ya ulinzi, Azam bado ina wanaume wa shoka. Ina Mzimbabwe, Bruce Kangwa, Waghana; Daniel Amoah na Yakubu Mohammed. Wote ni wanaume wa shoka na kazi yao uwanjani si ya kubeza.
Yakubu ndiye beki wa kati aliye bora zaidi nchini. Anamudu kucheza mipira ya juu na chini, ana kasi na anatumia akili kubwa katika kukaba. Ni ngumu kupita katika eneo lake. Kwa Ligi Kuu anakaribiwa uwezo na Method Mwanjali wa Simba.
Katika safu yao ya ulinzi bado Azam ina Aggrey Morris na David Mwantika, hao wote uwezo wao unafahamika. Aggrey si beki wa mchezo mchezo. Ukifanya tathmini ya kikosi cha Azam na namna wanavyocheza, ni wazi kwamba bado wana timu bora. Azam si timu nyepesi kama tunavyotaka kuamini. Natazamia watafanya kitu cha tofauti msimu huu.
Timu yao bado inacheza soka safi. Kocha Aristica Cioaba ana kombinesheni nzuri na muunganiko mzuri wa kiuchezaji. Timu inajenga mashambulizi kupitia pande zote.
Uzuri ni kwamba nahodha wa timu hiyo kwa sasa, Himid Mao, anaipenda kazi yake na anaifanya kwa umahiri. Himid ni kiongozi wa vitendo. Anapambana mwanzo mpaka mwisho wa mechi. Wachezaji wengine wanahamasika kupitia yeye.
* USISAHAU KULIKE PAGE YETU HAPA*
0 comments :
Post a Comment