KIPA CHELSEA ASEMA SANCHEZ AKITAKA NA AONDOKE ARSENAL KUNA MAJEMBE KULIKO YEYE
KIPA wa Chelsea, Thibaut Courtois, amesisitiza kwamba Klabu ya Arsenal inaweza kuachana na nyota wake, Alexis Sanchez, kwa kuwa pengo lake linaweza kuzibika. Courtois anaamini kuwa Arsenal wana wachezaji wengi wazuri ambao kwa ubora wao wanaweza kutumika kuziba pengo la nyota huyo raia wa Chile. Nyota huyo anafukuziwa na klabu ya Manchester City pamoja na Paris Saint Germain (PSG), ambayo ipo tayari kutoa kitita cha pauni milioni 35 ili kuinasa saini yake. Inadaiwa kuwa, Sanchez ana mpango wa kuhamia Manchester City, lakini huenda akabadili uamuzi huo endapo PSG watakuwa na mpango wa dhati kwa kuzidisha ada ya usajili. Sanchez (28), hakuwa katika kikosi cha Arsenal kilichocheza kwenye michuano ya Kombe la Emirates wiki iliyopita, ambapo kwenye posti yake ya Istagram alidai sababu za kukosekana alikuwa mgonjwa. Kutokuwapo kwake kumepunguza kidogo hali ya msuguano kuhusu hatima yake, huku kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, akisisitiza kwamba nyota wake huyo hauzwi. Mshambuliaji huyo, ambaye amefikisha mabao 72 katika kikosi cha Arsenal, anaweza kumaliza utata uliopo kwa kulazimisha usajili wa kwenda Manchester City. Alipoulizwa kuhusu Sanchez, Courtois alilieleza gazeti la Evening Standard kuwa Sanchez ni mchezaji bora kutokana na michezo yake aliyocheza msimu uliopita alionesha ubora mkubwa sana. “Sanchez ni mchezaji hodari mwenye uwezo mkubwa katika soka, mwepesi na mwenye mbinu, ni mchezaji muhimu kwao, lakini Arsenal wana wachezaji wenye ubora zaidi. “Watamkumbuka, lakini nafikiri wanaweza kupata mbadala bora zaidi yake na kwa kuwa tayari wamefanya usajili mzuri wa mshambuliaji,” alisema Courtois. Courtois, ambaye atakuwa kipa katika mchezo wa Kombe la Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal wiki ijayo, aliongeza kuwa angependa Sanchez asiwepo kwenye mchezo huo kutokana na ubora wake.
0 comments :
Post a Comment