MANCHESTER United imeanza Ligi Kuu England kwa kishindo ikiifumua West Ham United kwa mabao 4-0. Halafu unajua sasa nani aliyefunga mabao hayo? Mawili yametupiwa na straika kipande cha baba, Mbelgiji Romelu Lukaku aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Everton.
Mengine yalitupiwa kimiani na Anthony Martial na Paul Pogba, ila mabao ya Lukaku yalikuwa na maana kubwa kwani, yalithibitisha kuwa, Mashetani Wekundu walistahili kutokwa na Pauni 75 milioni (kama Sh213 bilioni za Kitanzania).
Katika pambano hilo Manchester wakiwa nyumbani walitandaza soka la nguvu, huku kila mchezaji akionyesha thamani yake sio kwa Lukaku ama Pogba tu, bali haya kwa Nemanja Matic ambaye alitua Old Trafford akitokea darajani Chelsea.
Achana na Manchester sasa hayo ni mambo ya Ulaya, tuizungumzie Simba ya Mcameroon Joseph Omog ambaye kwa aina ya wachezaji alionao mpaka sasa, alitakiwa kuwa mtu mwenye nyuso ya furaha wakati wote.
Omog na wasaidizi wake walipaswa kukunja nne kwenye benchi na kuhesabu mabao wakati timu yake inacheza.
Hata hivyo, bwana hali sio hali kwani licha ya kiwango kinachotandazwa na kikosi hicho, kuanzia mpira wa pasi na burudani, upande wa ulinzi nako kumetulia, huko kwenye kiungo ndio usiseme Haruna Niyonzima na wenzake wametisha mbaya.
Tatizo kubwa lipo kwenye safu ya ushambuliaji, ambapo katika dakika 450 safu hiyo imefunga mabao matatu tu, licha ya kuwa na wakali wa kufumaini nyavu kama Emmanuel Okwi, John Bocco ‘Adebayor’, Mrundi Laudit Mavugo na Juma Luizio, Nicholas Gyan kutoka Ghana na kina Shiza Kichuya na Mohamed Ibrahim.
TATIZO NINI
Hapa tunaizungumzia Simba yenye Okwi mwenye kasi, chenga na anajua kufunga, Mavugo mwenye nguvu na mashuti, Bocco mtaalamu wa mabao ya vichwa, lakini ushindi wake umekuwa mwembamba.
Kwa aina ya watu hao, ukisikia wamewapiga watu matatu, manne hakuna atakayeshangaa. Mbona Lukaku kaanza EPL na mabao yake mawili? Alexandre Lacazette ameshatupia Arsenal.
Neymar kule PSG kafanya yake, Simba tatizo nini?
Katika mechi tano walizocheza, mbili nchini Afrika Kusini na tatu hata Tanzania, Okwi na wenzake wametupia kambani mara tatu tu, moja alitupia Mo Ibrahim walipoicharaza Rayon Sport kwenye Simba Day.
Kisha akafuata Laudit Mavugo katika mechi ya kupimana ubavu mazoezini na Polisi Tanzania waliwafunga mabao 2-0 kabla ya juzi Jumapili Okwi kufunga bao pekee la kibahatibahati walipoivaa Mtibwa Sugar, kirafiki.
MIPANGO YA KOCHA
Kocha Omog amekuwa akiwatumia zaidi, Bocco na Okwi kuanza kwenye safu ya ushambuliaji baada ya kuwaona wanaelewana kiucheza kwa mfumo wa mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji wawili.
Iko hivyo pia, anapotumia mfumo wa mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu, mabadiliko anayoweza kufanya ni kuwaongezea straika mmoja na mara nyingi anakuwa Mavugo, ili Okwi acheze akitokea pembeni.
Mavugo, Luizio bado hawajapata nafasi ya kudumu ndani ya kikosi lakini bado kwa dakika chache wanazopewa kucheza, ndiyo nafasi yao kuhakikisha wanafanya kazi ya kueleweka na kupata nafasi ya kuanza kwa michezo mingine.
Kama iliweza kuingia ndani ya 18 kwa zaidi ya mara tano wakakosa mabao ya wazi katika mchezo wao wa kirafiki na Mtibwa Sugar wakamaliza kwa ushindi wa bao moja tu, endapo umakini utaongezeka, upo uwezekano wa kufunga mengi.
Mchezo huo ulikuwa wa tano wa kirafiki lakini hauna tofauti na mingine waliofungwa na Orlando Pirates 1-0, sare ya 1-1 na Bidvest Wits au ushindi wa 1-0 kwa Rayons ama walipoifunga Polisi Tanzania.
LAZIMA IJIPANGE
Kocha Omog amekuwa akipiga kelele, kwa aina ya wachezaji alionao ana kila sifa ya kusimama mbele ya watu na kutamba, lakini katika utendaji wanatakiwa kuonyesha wao ni wa aina gani, embu wapeni raha mashabiki wenu.
Matajiri wamewekeza na kufanya usajili wa maana, sasa wapeni raha mashabiki wenu, wanatembea kifua mbele timu ipo, lakini wanataka kumwona Okwi yule waliomsubiri kwa hamu kubwa anafanya yake Taifa, Bocco yule mtaalamu wa vichwa, wanatupia tu na hawakamatiki kama Lukaku.
NGAO YA JAMII
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja amekiri kuwa, safu yao imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi, lakini umaliziaji umekuwa mbovu.
Hata hivyo mewatoa hofu mashabiki wa Simba kwamba mechi yao ijayo ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga itakayopigwa Agosti 23 kwenye Uwanja wa Taifa, kila kitu kitakuwa sawa.
“Tunaendelea kurekebisha, tunaamini kutozoeana kwa wachezaji ni tatizo, lakini timu inazidi kuimarika na kabla ya kucheza na Yanga ama kuanza kwa Ligi Kuu tutakuwa tumeshatatua tatizo hilo la safu yetu ya mbele.
Straika Emmanuel Okwi naye amekiri kuwa, safu yao haijakaa vyema kwa vile wengi wa wachezaji ni wageni na ambao hawakaa pamoja kujua wanaocheza nao wanakitaka nini.
“Ila hata hivyo Yanga isijidanganye kwamba watapata mteremko, tukikaa vizuri tunaweza kuwapiga nyingi tu, sio wao bali hata klabu yoyote ya ndani ya nje ya nchi, makocha wanaendeela kutulisha mbinu na tunazoeana,” alisema Okwi.
Hata hivyo, Simba bado inapaswa kurekebisha mambo mapema, kwani kama itakutana na timu iliyo makini inaweza kuwatoa nishai kama walivyofanya Orlando Pirates ama Bidvest ambapo kiraka Erasto Nyoni alifunga bao na kuifutia aibu
0 comments :
Post a Comment