News
Loading...
Image Map HII NI 24 RADIO SIKILIZA NA UTUTUMIE SMS KWENDA 0684 666320 KUHUSU UNAVYOTUSIKIA

Saturday, 19 August 2017

MAKALA YA DOMO KAYA: SIMBA NA YANGA SISI TUNATAKA HIKI......HAYO MENGINE YA KWENU NYIE SIE HAYATUHUSU!!


NA WINFRIDA MTOI 

PAMBANO la watani wa jadi la Ngao ya Jamii, Simba na Yanga, linatarajiwa kupigwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Litakuwa ni pambano la aina yake kutokana na ukweli kwamba litavuta hisia za mashabiki wengi nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Pamoja na burudani wanayotarajia kupata mashabiki wa pande zote mbili, lakini mara nyingi katika pambano la watani kumekuwa kukijitokeza matukio mbalimbali ndani na nje ya uwanja.
Hiyo inatokana na presha ya mashabiki ambao wanakwenda uwanjani wakiwa na lengo moja la kuondoka na furaha ya ushindi.
Pambano la Agosti 23 litakuwa la nne kuwakutanisha watani hao wa jadi ambalo lilikuwa linaitwa Ngao ya Hisani, mara ya kwanza kucheza ilikuwa mwaka 2001 na Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Baada ya hapo ikasimama, wakaja kukutana tena mwaka 2010 ikiwa inaitwa Ngao ya Jamii na Yanga kushinda kwa mikwaju ya penalti 3-1, baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana. Mchezo mwingine ulikuwa 2011 ambapo Simba walishinda mabao 2-0.
Msisimko wa pambano la Ngao ya Jamii umezidi kuongezeka siku hadi siku, kitendo kinachoashiria kutakuwa na upinzani mkali.
Kuelekea katika pambano hilo, tayari kila timu imejichimbia kivyake licha ya kwamba klabu zote zimeelekea visiwani Zanzibar, Yanga wapo Kisiwa cha Pemba na Simba Unguja.
Tunajua kwamba timu hizo zimekwenda kuweka kambi visiwani humo kwa lengo la kufanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanaweka vikosi tayari kwa ajili ya mtanange huo ambao ndio ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tofauti na maandalizi hayo, inafahamika timu hizo zimefanya usajili wa wachezaji wapya wa kuongeza nguvu na kuziba mapengo yaliyoonekana katika msimu uliopita.
Simba inaonekana kufanya usajili mkubwa zaidi kwa kuchukua wachezaji wengi ambao ni nyota kuliko wapinzani wao Yanga ambao kipindi cha usajili walikuwa wanakabiliwa na ukata.
Hata hivyo, kulingana na utamaduni wa mechi za mahasimu hao wawili, licha ya usajili na vitu vingine bado presha inaendelea kuwepo ambapo kinachoangaliwa zaidi ni matokeo ya uwanjani pekee.
Desturi hiyo imekuwa ikisababisha mechi ya Simba na Yanga kuchezwa katika hali ya tofauti na michezo mingine, kwani mara nyingi hutawaliwa na ubabe, mabavu na kupoteza ladha halisi ya soka.
Tumezoea kuona mechi nyingi za Simba na Yanga zikikosa utulivu kuanzia uwanjani kwa wachezaji na waamuzi hadi mashabiki waliokaa jukwaani.
Ni kweli lazima mshindi apatikane, lakini timu zijaribu kucheza soka zuri la ushindani ambalo litamfanya mshindi apatikane kishujaa na kumpa raha shabiki aliyetoa fedha na kupoteza muda wake kupata burudani.
Timu zitakapocheza vizuri kwa kufuata sheria na kujiamini kwa maandalizi waliyofanya, yale mambo tunayoshuhudia kila mara kama vurugu zisizokuwa na mpango hazitajitokeza kipindi hiki.
Sawa wapo wale ambao wamezoea vurugu na wanakwenda uwanjani wakiwa wamejipanga, lakini naamini wengi wao wanakwenda kwa ajili ya kupata burudani ya soka na si vinginevyo.
Binafsi ninachoweza kusema ni kwamba klabu na mashabiki wajipange kuzishangilia timu zao ili waweze kupata burudani na matokeo mazuri
* USISAHAU KULIKE PAGE YETU HAPA*
Share on Google Plus

About

0 comments :

Post a Comment