HII NDIO SABABU YA KUPOKONYWA UNAHODHA MKUDE: GAZETI LAANILA KILA KITU 7-0 ZA SOUTH IKIWEMO!!
NA MWANDISHI WETU
BENCHI la ufundi la timu ya Simba likiongozwa na kocha, Joseph Omog, wamefanya mabadiliko na kumvua unahodha kiungo Jonas Mkude na nafasi hiyo kuchukuliwa na Method Mwanjali.
Ni mara chache sana kwa mchezaji kuvuliwa unahodha na kupewa mwingine, labda kwa suala la utovu wa nidhamu.
Hata kama mchezaji atakuwa chini ya kiwango ama kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza, havuliwi unahodha labda aamue kuondoka kwenye klabu hiyo ndio nafasi hiyo hupewa mwingine.
Lakini cha kushangaza, Omog na benchi lake la ufundi wamefanya mabadiliko hayo ya kumvua Mkude kitambaa cha unahodha na kumpa nahodha wa zamani wa Zimbabwe, Mwanjali bila ya kuwa na sababu za msingi.
Kwa mujibu wa mtandao wa Goal.com, umemkariri Omog, akisema: “Ni kweli nimefanya mabadiliko ambayo ni ya kawaida.”
“Hakuna kosa lolote ambalo Mkude amefanya ila ni mabadiliko yetu ndani ya timu na nina amini kila mmoja ameridhia na kazi itafanyika kwa umakini,” aliongeza Omog.
Chanzo cha habari cha gazeti dada na hili, Dimba, kimedai kwamba benchi la ufundi limeangalia kigezo cha busara na hekima ya Mwanjali uwanjani kwa kuwa Simba ina wachezaji wengi na wenye uzoefu mkubwa ndio maana wakaamua kumvua mkude kitambaa hicho cha unahodha.
Ni kweli Mwanjali ana hekima na ana uzoefu kwa kuwa alishawahi kuwa nahodha wa timu yake ya taifa.
Pamoja na Mwanjali, mwingine ni msaidizi wake John Bocco, naye ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa katika kuvaa kitambaa cha uhanodha kwa kuwa alikuwa nahodha wa klabu yake ya zamani ya Azam FC hadi anaondoka na pia amewahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Hivyo uamuzi wa kuwapa kitambaa hicho Mwanjali na Bocco wala si tatizo kubwa kwa kuwa wachezaji hao wameitumikia sana nafasi hiyo.
Lakini kama wameangalia nidhamu, uzoefu wa wachezaji hao kwanini nahodha wa tatu amekuwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ badala ya kubakia Mkude? Je, Tshabalala ameutoa wapi huo uzoefu wa kuweza kuunganishwa na ‘levo’ za akina Mwanjali na Bocco na Mkude aonekane hafai?
Hapo ndipo vigezo vilivyotumiwa na benchi la ufundi vinapokosa msingi wa maana na kuonyesha kwamba kuna kitu nyuma ya Mkude kuvuliwa unahodha.
Kama Mkude hana hekima zaidi ya Mwanjali ni kwanini waliamua kumpa unahodha huo badala ya wachezaji wengine waliokuwapo Simba kipindi hicho?
Wakati huo Simba ilikuwa na wachezaji wenye uzoefu kama mlinda mlango Vincent Angban, Jjuuko Murshid na Mwinyi Kazimoto.
Naamini wakati Mussa Hassan ‘Mgosi’ anaichezea Simba kwa mara ya mwisho na kukivua kitambaa cha unahodha na kumwachia Mkude, benchi la ufundi lilimwamini kiwango chake na ushawishi wake kwenye timu ndio maana waliridhia.
Hivyo kumvua kwa sababu nyepesi za hekima na nidhamu, hiyo inaonyesha wazi kwamba kuna kitu nyuma ya jambo hilo na benchi la ufundi limetumika.
Hakuna mwenye shaka juu ya kiwango cha Mkude, kwani ukweli uliowazi kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara hakuna kiungo mkabaji kama Mkude. Pia hakuna mwenye shaka juu ya uwezo wake wa kuhamasisha timu na kuweza kubadili matokeo.
Mechi kadhaa ambazo Mkude ameanzia benchi aliweza kuingia na kusaidia timu kubadilisha matokeo hata kama ilikuwa ngumu kwa kiasi gani, ikiwamo ile waliyoshinda mabao 2-1.
Kama ni masuala ya nidhamu basi kocha na benchi lake la ufundi angeweka wazi, hapo kusingekuwa na mtu wa kutilia shaka.
Lakini kwa sababu zilizotolewa ni wazi kwamba kuna kilichojificha nyuma ya pazia, kwani hata kusajiliwa kwa James Kotei kulikuwa na lengo la kumwondoa Mkunde, ambaye alidaiwa kuwasumbua viongozi wa Simba na kutaka alipwe shilingi milioni 70 ili asaini mkataba mpya.
Lakini kiungo huyo wa Ghana, Kotei alishindwa kumzima nyota huyo aliyetokea Simba B.
Mambo mengine yanayohusishwa na Mkude kuvuliwa unahodha inadaiwa kitendo cha kutoa siri kipigo cha bao 7-0 walizochapwa Simba nchini Afrika Kusini ni mojawapo.
Jambo ambalo linaweza likawa si kweli kwa kuwa kabla ya hilo, alishaletwa Kotei, ambaye pamoja na uwezo wake alishindwa kuonyesha umahiri kama wa Mkude.
Lingine linalodaiwa kuwa nyuma ya pazia ya kuvuliwa kwa unahodha huo ni kitendo cha Mkude kwenda kuchukua fedha yake ya kuongeza mkataba mpya kwa Mohammed Dewji, bila ya kupitia kwa ‘watu wa kati’.
Je, ni kweli hayo ndiyo yaliyojificha nyuma ya pazia au kuna nini kingine kilichosababisha Mkude avuliwe unahodha?
credit Bingwa
Duh! Hii habari haina kichwa wala miguu. Imeandikwa bila facts muhimu. Mwandishi ameingiza maoni yake kwenye suala la unahodha kwa lengo la kumtetea Mkude (labda ni rafiki yake) bila kuziangamiza uzito wa hoja za benchi la ufundi. Eti mchezaji akishapewa unahodha hapaswi kuvuliwa! Hii mpya! Halafu hilo suala la 7-0 limezungumzwa lakini lina-hang. Mwandishi anataka kuwaaminisha wasomaji ni kweli Simba ilicheza mchezo wa kirafiki na kufungwa idadi hiyo ya magoli wakati anaujua ukweli. Ameingiza uzushi wa mitaani kwenye habari. Mhariri aliyepitisha habari hii hakuwa makini.
ReplyDelete