MAKAMU Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga,Clement Sanga, amefunguka na kuweka wazi sababu za uongozi kutomsajili winga wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa.
Sanga alisema alishangazwa na taarifa zilizoenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii juzi zikidai kuwa,Yanga wamerudisha Ngassa katika kikosi chao.
“Hakuna ukweli wowote kuhusu Ngassa kusajiliwa na Yanga, kwa ufupi Yanga haimhitaji Ngassa na hakuwepo katika mapendekezo ya kocha George Lwandamina,” alisema Sanga.
Alisema ilikuwa ni vigumu Wanajangwani hao kumsajili Ngassa kwani katika ripoti ya msimu uliopita ya kocha Lwandamina,hakuna sehemu aliyopendekeza winga huyo asajiliwe.
“Hatuwezi kumsajili mchezaji ambaye hakuwepo katika mipango ya mwalimu, hivyo tumesajili kulingana na matakwa ya kocha na si mtu mwingine, kwa hiyo Ngassa hakuwa na nafasi,” aliongeza Sanga.
Kwa muda mrefu Ngassa amekuwa na shauku kubwa ya kutaka kurejea katika kikosi cha Yanga licha ya kushindwa kufanya vizuri akiwa na timu za Mbeya City na Free State Star ya nchini Afrika Kusini.


0 comments :
Post a Comment