UKIHESABU mchezaji mmoja mmoja, Simba inaweza kuwa ndiyo timu iliyosajili wachezaji maarufu na wenye uzoefu mkubwa kuliko timu nyingine za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Imeachana na wachezaji kumi na kusajili wengine 14 kutoka nje na ndani ya Tanzania.
Baadhi ya mastaa waliosajiliwa ni pamoja na Mganda Emmanuel Okwi ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi, John Bocco, Shomari Kapombe, Ally Shomary, Aishi Manula na Said Mohammed ‘Nduda’.
“Kiujumla usajili tulioufanya ni mzuri na viongozi wamefanikiwa kuniletea aina ya wachezaji ninaowahitaji ili timu iweze kufanya vizuri msimu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni,” anasema kocha wa timu hiyo Mcameroon Joseph Omog.
“Nimepata kundi kubwa la wachezaji wazoefu, waliopevuka na wenye kiwango kizuri, ambao bila shaka watakuwa na mchango mkubwa kwa timu katika mashindano mbalimbali ambayo tutashiriki msimu ujao.
“Matarajio yetu ni kufanya vizuri ambako si kwa namna nyingine bali kutwaa ubingwa kwenye kila mashindano ambayo tutashiriki. Kiu ya mashabiki na kila mmoja ni kutaka kuona timu inapata mafanikio ya kuchukua kombe na si vinginevyo. Msimu uliopita tulifanikiwa kuchukua Kombe la FA tu lakini hatukufanikiwa kubeba lile la Ligi Kuu.
“Kwa ubora wa kikosi cha Simba hivi sasa, kipaumbele cha kwanza ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ambao hatujafanikiwa kuuchukua kwa kipindi kirefu, pia tumepanga kutetea ubingwa wa Kombe la FA sambamba na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
“Kambi zote mbili (Afrika Kusini na Unguja) zimekuwa na mafanikio kwetu kwa sababu utulivu uliokuwepo umewasaidia wachezaji kuelekeza akili zaidi kwenye programu za mazoezi na kuwa sawa kisaikolojia, jambo ambalo litakuwa na faida kwa timu.
“Kupitia kambi hizo tumepata nafasi ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza msimu uliopita, hivyo naamini tutaingia kwenye ligi tukiwa tayari kuikabili vita iliyo mbele yetu.
“Ligi itakuwa ngumu kwa sababu nimesikia timu nyingi zikifanya usajili mzuri na kuanza maandalizi mapema. Na ugumu huo hasa utakuwa kwetu kwa sababu timu nyingi zimekuwa zikikamia sana pindi zinapokutana na Simba na ukiongeza na huu usajili tulioufanya, tutakuwa na vita kubwa.”
Yanga na Kimataifa
Akiwazungumzia wapinzani wake wakubwa hao, Omog anasema:
“Yanga ni timu nzuri ambayo kikosi chake hakijafanyiwa mabadiliko makubwa, hivyo naamini watakuwa tishio. “Nimekuwa nikifuatilia mechi zao, kikubwa kinachowabeba ni kuwa na wachezaji wanaojituma na wenye nidhamu ya kupambana na kufuata maelekezo kwa muda wote wa mechi.
“Ukiwa na timu yenye wachezaji wanaojituma na kujitambua inakuwa ni faida kwa timu jambo ambalo linawasaidia Yanga. Hata hivyo siwaogopi, nawaheshimu kama ninavyoziheshimu timu zote zilizo Ligi Kuu.
“Kuna miezi sita imebaki kabla ya kuanza kwa mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu, hivyo ni mapema mno kuanza kuzungumzia mashindano hayo wakati kuna ligi na Kombe la FA ambayo tunatakiwa kufanya vizuri.
“Hata hivyo kama nilivyosema awali kwamba mkakati wetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye kila mashindano.
“Hili litatimia tu iwapo wachezaji watakuwa na nidhamu, juhudi na malengo.”
YANGA AFRICANS
JUMAMOSI Ligi Kuu inaanza Bongo. Hata hivyo, bado wasiwasi wa mashabiki upo kwa Yanga kutetea ubingwa wao huku kura nyingi zikiangukia kwa Simba na Singida United.
Usajili usio na mbwembwe iliofanya Yanga safari hii umeonekana hata kuwapa wasiwasi mashabiki wa klabu hiyo, kwani ni jambo ambalo hawajalizoea kutoka kwa kamati ya usajili ya klabu hiyo.
Kwa miaka ya karibuni tumeshuhudia Yanga ikitikisa katika anga za usajili kwa kusajili mchezaji yoyote waliyemtaka iwe ndani au nje ya nchi lakini safari hii mambo yamekwenda tofauti, wengine wakidai labda kutokana na uchumi wa klabu hiyo kuyumba kwa sababu aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji kakumbwa na misukosuko.
Usajili mpya
Yanga imesajili wachezaji tisa tu msimu huu kutoka klabu mbalimbali wakiwemo Ibrahim Ajib-Simba, Abdallah Haji Shaibu (Taifa Jang’ombe Zanzibar), Pius Buswita (Mbao), Youthe Rostand (African Lyon), Burhan Akilimali, Ramadhan Kabwili (Serengeti Boys), Raphael Daudi (Mbeya City), Gadiel Michael(Azam) na Papy Kabamba Tshishimbi aliyetokea Mbabane Swallows ya Swaziland. Yanga imejitahidi kusajili kwa kuzingatia mapungufu ya kikosi chake ikiwemo kutafuta kiungo mkabaji ambaye ni Tshishimbi baada ya nafasi hiyo kuwasumbua kwa muda mrefu, pia Gadiel ameziba nafasi ya Oscar Joshua aliyeachwa, hivyo atasaidiana na Haji Mwinyi katika beki ya kushoto wakati Raphael Daud akichukua nafasi ya Haruna Niyonzima aliyetimkia Simba.
Beki wa Kati bado tatizo
Licha ya kumsajili Abdallah Shaibu’Ninja’ kutoka Taifa Jang’ombe, safu ya ulinzi ya Yanga imeonekana bado haijatulia kwani pamoja na kuwa na wazoefu kama Nadir Haroub’Cannavaro’, Kelvin Yondani na Andrew Vincent bado imekuwa ikiyumba.Kuondoka kwa Vincent Bossou kumeonyesha upungufu kwenye safu ya ulinzi ya Yanga kwani katika mechi za kirafiki imeonekana kutotulia ingawa hata hivyo, bado mabeki wana muda wa kujirekebisha na kucheza vizuri. Viongozi wa klabu hiyo walijitahidi dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa kutafuta beki mmoja wa kimataifa lakini jitihada zao ziligonga mwamba kwani kila waliyemleta kwa majaribio alionekana hayupo katika kiwango bora, lakini baadae ikajulikana hata kama ingempata beki wa kati, isingeweza kumsajili kwani kanuni zinawabana na walikuwa wamechelewa.
Hata hivyo, kocha na mnazi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amewaambia mashabiki wa Yanga ana imani na Cannavaro na Yondani na Yanga itakuwa imara tu.
Hali ya kifedha
Viongozi wa Yanga mara kwa mara wamekiri hali ya uchumi ya klabu imeyumba lakini bado wamejipa moyo haiwazuii kutwaa ubingwa msimu ujao.
Matatizo ambayo yalimpata aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuph Manji hivi karibuni yemeivuruga klabu kwa kiasi kikubwa kwani ndiye alikuwa nyuma ya mafanikio ya timu hiyo kutokana na kutoa fedha zake kwa ajili ya kambi na mishahara ya wachezaji.
Misimu miwili iliyopita Yanga ilikuwa ikiweka kambi nje ya nchi wakati wa maandalizi ya msimu ikiwemo kwenda nchini Uturuki lakini safari hii kutokana na uchumbi kuyumba, ikaanzia maandalizi yake ya ligi mkoani Morogoro kabla ya kutimkia Pemba kujiandaa na mechi ya Simba.
Je ina kikosi cha ubingwa?
Bado Yanga ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa licha ya wengi kuona haijafanya usajili wa maana msimu huu.
Timu hiyo imefanya usajili wa kuzingatia maeneo yatakayowabeba licha ya kupungua nguvu kidogo hasa kutokana na kutokuwepo kwa winga Simon Msuva aliyechangia kwa kiasi kikubwa ubingwa wa timu hiyo.“Yanga ina nafasi kubwa ya ubingwa kwa sababu bado ina timu nzuri, lakini ukweli kutokuwepo kwa Msuva ni pengo kubwa kwa Yanga kwani alichangia asilimia 70 ya mabao yote ya Yanga msimu uliopita, hivyo hii ni changamoto kwao msimu huu kwani sidhani kama katika usajili wao kuna mchezaji anaweza akaziba pengo lake,” anasema Ally Mayay.
Wapinzani Simba na Singida United
Yanga inafahamu katika mbio zake za kutetea ubingwa itakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Simba na Singida United hivyo ni lazima ijipange kwa hilo. Hata hivyo, ni wazi uzoefu wa wachezaji wengi wa Yanga utaibeba timu hiyo. Licha ya Simba kusajili mastaa na kuonekana itatoa upinzani lakini bado ugeni wa wachezaji wake wengi katika kikosi hicho cha Kocha Joseph Omog unaweza ukaikwamisha mbele ya Yanga yenye wachezaji wengi waliokaa pamoja muda mrefu. Pia hata Singida United pamoja na kuonekana itawapa Yanga ushindani lakini bado kuna usemi unaosema mkubwa ni mkubwa tu na ndio maana hata katika mchezo wa kirafiki ambao timu hizo zilikutana hivi karibuni, Yanga ilitoka nyuma kwa mabao mawili na kupata ushindi wa jioni wa mabao 3-2.
* USISAHAU KULIKE PAGE YETU HAPA*
0 comments :
Post a Comment