SIMBA juzi walianza kuhesabu mataji baada ya kutwaa Ngao ya Jamii ikiifunga Yanga kwa penalti 5-4 katika pambano lililopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, lakini gumzo la mechi ni soka la kiungo mpya wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi.
Rasta huyo alipiga soka la uhakika licha ya ugeni wake ndani ya kikosi cha Yanga na haikuwa ajabu kuvuna alama nyingine miongoni mwa nyota waliocheza jana.
YANGA:
Youthe Rostand- 7
Yanga haikufanya makosa kumsajili Mcameroon huyo kwani, alikuwa kizingiti kwa nyota wa Simba na aliokoa penalti ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Aliwapanga vema mabeki wake na kuokoa krosi tano za hatari ambazo zingeweza kuzaa mabao.
Juma Abdul- 6
Alikuwa mzito tofauti na alivyozoeleka ndio maana Emmanuel Okwi alimsumbua kiasi chja kumchezea vibaya Mganda huyo na kupewa kasi ya njano dakika ya 37 na kutolewa kumpisha Hassan Kessy.
Gadiel Michael- 8.5
Aliwanyima raha Simba upande wao wa kulia kutokana na kasi yake na uwezo wa kupokonya mipira kutoka kwa washambuliaji jambo lililowafanya Okwi na Kichuya wabadilishane nafasi kila wakati uwanjani.
Kelvin Yondani-8
Ameendelea kuwa mtu muhimu katika safu ya ulinzi ya Yanga kwa hesabu zake kali za kuwakabili washambuliaji wa timu pinzani. Jana aliwachunga vyema kina Niyonzima, ingawa alikuja kukosa penalti ya kwanza ya Yanga.
Andrew Vincent-7.5
Alikosa utulivu mara kadhaa jambo lililosababisha afanye makosa yaliyowapa faida Simba, lakini uwepo wa Yondani na kipa Rostand ulificha makosa yake.
Kabamba Tshishimbi-9
Licha ya ugeni wake kikosini Yanga, kiungo huyo alikuwa hodari wa kupokonya mipira kutoka kwa viungo wa Simba na pasi zilifikia walengwa na aliwapa kazi ngumu viungo wa Simba kabla ya kufunga penalti maridadi.
Ibrahim Ajibu-7
Hakuonyesha makali yaliyotegemewa na wengi, japo dakika ya 29 alifanya kazi ya ziada kumtoka Method Mwanjali na kupiga krosi ambayo kama sio uhodari wa Aishi Manula, Yanga ingeweza kufunga bao. Pia alifunga penalti murua kabisa.
Thabani Kamusoko-8
Aliweza kuiunganisha vyema timu na kuisogeza mbele hasa kutokana na staili yake ya kutawanya mipira sehemu mbalimbali za uwanja.
Pasi sake ndefu kwenda sehemu za pembeni, ziliwapa tabu mabeki na viungo wa Simba na kuwafanya wasipande mara kwa mara.
Donald Ngoma-7
Uwezo wake wa kumiliki mpira, kasi na nguvu, vilimpa wakati mgumu Method Mwanjali aliyejikuta akizawadiwa kadi ya njano dakika ya 11 kwa kumuangusha.
Aliwachosha mabeki wa Simba ambao walilazimika kumchezea rafu za mara kwa mara. Naye alifunga penalti yake.
Rafael Daud-7
Alicheza kama kiungo wa nyuma ya mshambuliaji ambapo, jukumu lake lilikuwa ni kutengeneza nafasi za mabao na kuchezesha timu.
Alipiga pasi kadhaa kwenda kwa mastraika wa Yanga lakini nyingi hazikutumiwa vyema kuipatia timu hiyo bao.
Emmanuel Martin-7
Kasi yake ilimfanya beki Ally Shomary asipande mbele mara kwa mara na kuifanya Yanga iwe imara zaidi kwenye upande wake wa kushoto.
Mara kwa mara alirudi kumsaidia Gadiel Michael jambo ambalo lilimfanya Shiza Kichuya asiwe analeta madhara kwenye lango lao.
SIMBA:
Aishi Manula-8
Aliokoa michomo kadhaa iliyoelekezwa langoni mwake, hasa krosi ya Ibrahim Ajibu dakika ya 29 na shambulizi la Emmanuel Martin dakika ya 78.
Aliokoa penati ya kwanza ya Yanga iliyopigwa na Kelvin Yondani.
Ally Shomary-7
Dakika 15 za mwanzoni, zilikuwa nzuri kwake kwa kupanda mara kwa mara na kupiga krosi ambazo zingeweza kuzua kizaazaa lakini baadaye alianza kuelemewa na kasi ya Emmanuel Martin jambo lililomfanya aache kupanda.
Erasto Nyoni-7
Alikuwa na utulivu katika kumdhibiti Ibrahim Ajibu na alifanikiwa katika hilo kwani, mshambuliaji huyo wa Yanga hakuweza kuonyesha makeke yake kama ilivyotegemewa.
Salim Mbonde-8
Ilikuwa ni mechi yake ya kwanza ya watani wa jadi, ila alicheza vyema akiokoa mashambulizi mengi ambayo yalielekezwa langoni mwa Simba hasa mipira ya juu ambayo alikuwa akipewa Donald Ngoma.
Method Mwanjali-8
Aliwaongoza vyema wenzake hasa wale wa safu ya ulinzi ambayo jana ilikutana na shughuli ya washambuliaji wa Yanga, japo alikutana na ugumu mbele ya Ngoma. Alifunga penalti ya kwanza.
James Kotei-7
Alipata wakati mgumu mbele ya Kamusoko na Rafael, lakini alipambana vilivyo kuhakikisha mabeki wake wanakuwa salama.
Shiza Kichuya-7
Alihaha huku na kule kujaribu kuleta madhara langoni mwa Yanga, lakini Gadiel Michael alifanikiwa kupambana naye dakika zote tisini za mchezo. Alifunga penalti yake kiufundi.
Muzamiru Yassin-6.5
Ufundi wa Tshishimbi kwenye safu ya kiungo ya Yanga, ulimpoteza Muzamiru ambaye hakuweza kabisa kuonyesha makali yake kwenye mchezo huo.
Laudit Mavugo-6
Alipoteza nafasi nne za mabao ambazo alitengenezewa na wachezaji wenzake ambapo, vichwa vyake vitatu vilitoka nje ya lango huku shuti lake moja nalo likishindwa kulenga lango, japo aliwapa ugumu mabeki wa Yanga kukosa uhuru.
Emmanuel Okwi-6.5
Alimsumbua vilivyo Juma Abdul upande wa kushoto na kumzuia kupanda mbele, japo alichoka kipindi cha pili na ni mmoja ya waliofunga penalti.
Haruna Niyonzima-6
Alihaha kujaribu kutengeneza nafasi za mabao, lakini alikutana na ukuta mgumu wa Yanga uliokuwa chini ya Tshishimbi. Pasi zake nyingi zilifikia walengwa na alionyeshwa kadi kipindi cha pili kwa kumchezea rafu Juma Abdul. Alifunga moja ya penati za simba
0 comments :
Post a Comment