MASHABIKI wa Yanga wanahesabu saa tu kuanzia leo Jumanne kabla kiungo wao mpya, Papy Tshishimbi Kabamba, hajasaini mkataba wa kujiunga na timu yao, huku baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wakianza kuwapiga kijembe watani zao, Simba.
Viongozi hao wamedai kuwa ujio wa Kabamba utakifanya kikosi chao kuwa na marasta wawili eneo la kati ambao kwa soka la nguvu wanalocheza, ni wazi Simba watakaovaana nao Agosti 23 katika mechi ya Ngao ya Jamii lazima waombe po!
Simba na Yanga zitavaana katika mchezo huo wa kufungua msimu mpya wa 2017-2018 huku klabu zote zikitoka kuimarisha vikosi vyao kupitia dirisha la usajili linaloendelea mpaka Agosti 6.
Yanga imepata kiburi zaidi baada ya ujio wa Kabamba ambaye anatokea klabu ya Mbabane Swallows ya Swaziland, ambayo iliitoa Azam katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutinga hatua ya makundi kabla ya kukwamia huko.
Sababu ya Yanga kuanza kuwatambia Simba mapema ni jinsi Kabamba anavyotua katika kikosi chao kudhibiti eneo la kati, akiwa rasta kama ilivyo kwa fundi wao mwingine Thabani Kamusoko anayetokea Zimbabwe.
Kamusoko aliyesajiliwa Yanga miaka miwili iliyopita akitokea FC Platnum ya kwao, ni kati ya nyota waliofunika nchini katika Ligi Kuu Bara ambapo Yanga ilitwaa mataji mawili na lile la Kombe la FA walilopokwa msimu uliopita na watani zao hao, Simba.
“Kama Kamusoko tu aliwanyamazisha, itakuwaje akiwepo tena kikosini rasta mwingine mkali, yaani hapa rasta kule rasta, Simba wanatokaje kwa mfano?” Alihoji mmoja wa wajumbe wa Yanga, ambao baadhi yao walihudhuria mazoezi ya jana Jumatatu asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, ingawa rasta Kabamba hakuwepo kabisa akifichwa hotelini ili amalizane kwanza na mabosi wa klabu hiyo.
Kamusoko ambaye msimu wake wa kwanza tu aliifungia Yanga mabao matano, ni mmoja kati viungo waliotikisa Ligi Kuu kwa misimu hiyo miwili akiwa mahiri kwa kukaba, kupeleka mashambulizi mbele sambamba na kupiga pasi zenye macho.
Ufundi kama huo ndio alionao Kabamba aliyeonyesha mpira mwingi kwenye mechi dhidi ya Azam liliyopigwa mapema mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
KIBERENGE, MNIGERIA
Katika mazoezi hayo ya jana yaliyosimamiwa kikamilifu na Kocha George Lwandamina na watu wake wa benchi la ufundi, nyota wapya wa Yanga akiwamo Henry Tony Okoh kutoka Nigeria na Mkameruni Fernando Bongyang walishiriki tizi hilo sambamba na kiberenge kipya, Burhan Yahya Akilimali na wengine.
Akilimali alionyesha kwanini aliivutia Yanga imchukue kutokana na kasi na uwezo mkubwa kisoka alionao, huku Mnigeria alithiubutisha amekujka Yanga kusaka nafasi kwa jinsi alivyokuwa akikaba kwa umahiri kama alivyofanya Bongyang.
Kocha Lwandamina aliwapigisha mazoezi ya kumiliki mpira na kufungua vyumba, ambapo wachezaji walifanya kwa ufasaha na kumfurahisha Mzambia huyo.
MSIKIE KABAMBA
Rasta Kabamba, akizungumza na TANZANIA HOT NEWS aliwaambia mashabiki wa Yanga kwamba wasipate shida kutamka majina yake na kwamba jina rahisi kwao wamuite ‘Papii’, lakini akawaambia mara atakaposaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo atafuta kiu yao ya matatizo ya kiungo mkabaji na akicheza hapo hata Haruna Niyonzima afike tu na Simba yake amuonyeshe kazi.
Kabamba alisema anafahamu upinzani wa Simba na Yanga, lakini ukweli ni kwamba yeye anamudu kucheza nafasi zisizopungua saba uwanjani, lakini kocha Lwandamina akimpa jukumu katika kiungo mkabaji hapo ndipo huwa mtamu zaidi.Alisema anapokuwa uwanjani akicheza kiungo mkabaji huwa hachoki na jukumu lake kubwa ni kukaba kwa nguvu na kwa juhudi kubwa sambamba na kuanzisha mashambulizi.
Kabamba alisema mbali ya ubora huo, pia anapopandisha mashambulizi amekuwa akifunga mabao na alipokuwa Mbabane aliifungia mabao matatu katika Kombe la Shirikisho msimu huu.
0 comments :
Post a Comment